
Annual General Meeting of the Crop Science Association of Tanzania (CROSAT)
December 2, 2022
CROSAT Launches its Constitution
May 4, 2024Chama cha Taaluma ya Sayansi ya Kilimo Mazao Tanzania (CROSAT) kiliundwa kwa lengo la kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wanaojihusisha na kilimo mazao Tanzania ili kupeana mawazo, kushirikishana ujuzi na uzoefu kuhusiana na Kilimo mazao ili kuinua sekta hii na kuchangia maendeleo ya kiuchumi. Wanachama wa CROSAT ni wanasayansi, wakufunzi, watafiti, wakulima, wajasiriamali, makampuni, mashirika yasiyo ya kiserikali, maafisa kilimo, wanafunzi na wadau wote wanaojihusisha na kilimo mazao.
Wanachama wa CROSAT hukutana kila mwaka kwa ajili ya mkutano mkuu (AGM) ambao hutumika kujadili masuala yanayowahusu. Desemba 2023, CROSAT ilifanya mkutano mkuu wa mwaka katika hotel ya Morena, mkoani Dodoma. Mkutano huu ulikuwa na kauli mbiu isemayo “Kuijenga Kesho Iliyo Bora; Mfumo Bora wa Mbegu and Matumizi Salama ya Viuatilifu kwa ajili ya Kilimo Endelevu”

Wanachama wa CROSAT katika Mkutano Mkuu, Dodoma 2023
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano, Prof. Kallunde Sibuga ambaye ni Rais wa CROSAT aliwapongeza wanachama kwa kuhudhuria na kuwataka kuendelea kuwa wanachama hai ili kutimiza malengo ya CROSAT. “Ni shauku yangu kama Rais wa kwanza wa CROSAT kuona CROSAT ikiwa Chama chenye nguvu ambacho wanachama wake watajitoa na kuwa tayari kutumia ujuzi wao kuleta mabadiliko kwenye maendeleo na matumizi ya Sayansi kilimo na kuchangia Ukuaji wa Uchumi na Taifa Endelevu”

Rais wa CROSAT, Prof. Kallunde Sibuga akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka 2023
Katika mkutano huo wanachama walipata fursa ya kujadili na kupitisha mambo mbalimbali ikiwemo mpango mkakati wa chama, bajeti ya mwaka pamoja na kupitisha Katiba ya Chama hicho.
Sambamba na hayo, mkutano wa CROSAT uliambatana na semina ambayo ilitolewa na wazungumzaji wakuu wafuatao; Prof. Maulid Mwatawala ambaye ni Makamu wa Mkuu wa Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) – Taaluma, ambaye alizungumza umuhimu wa utambuzi sahihi wa wadudu waharibifu katika Soko la kimataifa. Mwingine ni, Prof. Joseph Ndunguru ambaye ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), ambaye alizungumzia umuhimu wa Bioteknolojia katika kutambua magonjwa ya mimea kwa Urahisi. Pamoja na Mr. Patrick Ngwediagi ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) yeye alizungumzia matumizi ya mbegu Bora, na Prof. Elininganya Kweka ambaye ni Meneja katika kitengo cha Ubora wa Viuatilifu TPHPA aliyezungumzia matumizi sahihi ya Viuatilifu.
Katika mkutano huu makampuni pia yalipata fursa ya kufanya mawasilisho ambapo kampuni ya CORTEVA Agriscience pamoja na SEEDCo walizungumza kuhusiana na huduma wanazozitoa hususan pembejeo za kilimo na mbegu bora mtawalia.
Pamoja na hayo wakulima na wazalishaji mbalimbali walipata fursa za kuonyesha bidhaa zao na kushirikishana uzoefu na wanachama wengine. Washiriki wa mkutano walipata fursa ya kutoa maoni yao kuhusu nini kifanyike kuboresha uzalishaji na kuwaletea maendeleo. Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa kwa kina ni kuhusu matumizi ya viuatilifu, matumizi ya mbegu, pamoja na upatikanaji wa masoko.

Mkulima na mwanachama wa CROSAT, Brig.Gen.(Mst.) Damian Mwanjile akitoa zawadi ya korosho.

Mkulima na mzalishaji wa mbegu, Mr. Kizito akionyesha baadhi ya mbegu anazozalisha kwa Mgeni Rasmi
Katika kuhitimisha mkutano huu wanachama walikumbushwa kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa CROSAT na kutumia akili na maarifa waliyonayo kayika kukuza kilimo mazao na kuchangia maendeleo ya Taifa. Mwisho wa semina hii uliweka mwanzo wa maandalizi ya semina nyingine ambapo kwa mwaka 2024, CROSAT inatarajia kuwa na Mkutano Mkuu ambao utaambatana na Semina ya Kisayansi.

Baadhi wa washiriki wa mkutano mkuu wakifuatilia mkutano kwa karibu

Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu 2023 katika picha ya Pamoja